Maaskofu Walaani Mauaji ya Polisi na Utekaji Wananchi
Matukio
ya utekaji watu na kupotea kwenye mazingira yasiyoeleweka pamoja na
mauaji ya polisi wanane mkoani Pwani, ni baadhi ya mambo yaliyotawala
katika mahubiri ya mkesha na ibada za Sikukuu ya Pasaka katika maeneo
mbalimbali nchini.
Maaskofu,
wachungaji na mapadri wa makanisa mbalimbali katika ibada zao,
walitumia muda mwingi kuzungumzia matukio hayo na kutahadharisha kuwa ni
ishara mbaya ya kuporomoka kwa amani nchini.
Viongozi
hao wa dini wanayatazama matukio hayo kwa sura mbili, kwamba yanafanywa
na binadamu walio hai na binadamu wafu ingawa ni hai.
Askofu Amani-Moshi
Katika
mahubiri yake, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi mkoani
Kilimanjaro, Isack Amani, alisema vitendo vya utekaji nyara, biashara ya
binadamu, mauaji ya askari, ubakaji na ulawiti na mengine yanayofanana
na hayo, ni dalili ya amani na utulivu wa nchi kupotea.
Akihubiri
katika ibada ya Pasaka iliyofanyika kitaifa katika Kanisa la Askofu la
Kristo Mfalme, mkoani Kilimanjaro, Askofu Amani alisema vimekuwapo
vitendo vingi vya uhalifu vinavyoendelea kutokea nchini yakiwamo mauaji
ya ukatili ya askari, utekaji nyara na unyanyasaji wa raia, hali
inayoonyesha kupotea kwa amani na utulivu nchini.
“Sasa
majambazi wamefikia hatua ya kuua askari, hii ni ishara mbaya na wapo
baadhi yetu wanashangilia. Inaonyesha kwamba ni makundi mabaya ya
uhalifu tuliyo nayo kwenye jamii.
“Kwa lugha nyingine tunaweza kusema tunahitaji msaada kwa sababu hali si nzuri na inatishia amani, umoja na utulivu wetu.
“Amani
na utulivu ni vitu ambavyo vinapaswa kuchochewa kama moto ila sasa
naona mambo hayako sawa. Ni lazima wananchi pamoja na Serikali yetu
tubadilike, tuichochee amani yetu,” alisema Askofu Amani.
Alisema
pia kwamba kuendelea kufanyika biashara haramu ya binadamu ni jambo
jingine linaloonekana kuchangia kuongezeka vitendo vya uhalifu.
“Biashara
haramu ya biandamu huliingiza taifa lolote kwenye maafa mengi ya
uhalifu kwa vile watu wamekuwa wanakodishwa na kufanya uhalifu. Hivyo
basi, ni lazima Watanzania tubadilike na kuishi maisha yenye staha.
“Mauaji
ya vikongwe na watu wenye ualbino, ushirikina, chuki, ubinafisi na
kulipiza visasi ni baadhi ya mambo yanayoonekana kuidhoofisha nchi,
hivyo ni lazima Serikali na wananchi wabadilike kulinda amani na
utulivu.
“Wananchi
tuungane na Serikali kulaani mambo yote ya uhalifu yanayoendelea
nchini, tuliombee taifa letu ili wananchi tuwe na umoja katika kupambana
na matendo ya uhalifu na uovu wote, na mkumbuke amani ya taifa letu ipo
mikononi mwetu,”alisema.
Askofu
huyo aliwataka wanasiasa wote nchini, waache ubinafsi kwa kufanya kazi
za kuimarisha vyama vyao pekee na badala yake watumie muda huo
kuwaletea wananchi wao maendeleo.
Katibu Mkuu -TEC
Katibu
Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Padri
Raymond Sabba, alisema taifa linatakiwa kuombewa ili kuondokana na
matatizo katika kipindi hiki cha mashaka ili mambo yanayojitokeza
yasiendelee kutokea.
Akihubiri
wakati wa mkesha wa Pasaka katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph
Dar es Salaam, Padri Sabba alisema kwa kiasi kikubwa yanayoendelea
yanatakiwa kukemewa.
Alivitaja
vitendo hivyo kuwa ni pamoja na mauaji ya kutisha, watu kutekwa nyara,
ufisadi, uzembe wa viongozi, dawa za kulevya na kukosekana kwa haki.
"Tuliombee
taifa katika kipindi hiki ambacho inawezekana kumekuwa na mashaka
yakiwamo mauaji ya ajabu kwa watu wasio na hatia kama albino, vikongwe
na kukosekana kwa haki.
“Kila
mtu anapaswa kutambua kuwa hayo yote ni makaburi yanayopaswa kuondolewa
kwa sababu hayampendezi Mungu kwa vile pia yanadhalilisha utu wa
mtanzania.
“Wanaotenda
matendo hayo wakati mwingine si wapagani bali ni wenye dini
wanaojitambulisha kuwa ni wakristo wakati matendo yao hayafai,” alisema Padri Sabba.
Aliwataka
wakristo kuhakikisha wanaliombea taifa katika kipindi hiki ambacho kuna
mashaka juu ya mambo mbalimbali ya kutisha yanayoendelea nchini.
Askofu Sylvester Gamanywa
Askofu
wa Kanisa la BCIC lililoko Mbezi Beach, Dar es Salaam, Sylvester
Gamanywa, alisema matukio yanayotokea nchiniyana sura mbili.
“Hayo
yanafanywa na binadamu walio hai na binadamu wafu ingawa ni hai. Kwa
kifupi, yanafanyika mambo ya ajabu na ya kusikitikisha na ya kuudhi
wakati mwingine.
“Huwezi
kutoa uhai wa binadamu kama kitu cha mchezo. Tumeshuhudia mauaji ya
polisi waliouawa Kibiti na si hao tu wameshauawa wengi. Tusishangae hayo
ni matendo ya watu waliokufa kiroho.
“Kwa mateso aliyoyapata Yesu, tungeweza kuua askari wote kwa mkupuo, lakini Yesu badala ya kuua, alisamehe.
“Unapoona watu wanafanya vituko, mfano wazee wanafanya zinaa na watoto waliowazaa, hao ni wafu, wamekufa kiroho.
“Mara nyingi kifo cha roho huanzia kwenye kinywa cha mtu ambako maneno yake yanaweza kutoa majibu kama ni hai au mfu.
“Kama
mtu anatoa maneno ya chuki, fitina, uchonganishi ama kupandisha watu
hasira, hizo ni dalili za mauti ndani ya kinywa chake,” alisema Gamanywa.
Alisema
pia kwamba licha ya kuwapo kwa mamlaka za dola nchini, bado mambo
mengi yanayotendeka kwenye jamii yanadhihirisha mamlaka zimezidiwa
kutokana na kuongezeka kwa maovu kuliko nguvu ya udhibiti iliyopo.
“Mfu
wa roho yuko hai mwili, lakini utashi wa kufufuka ni hiyari yake
mwenyewe. Majambazi, wazinzi, waongo na wachawi, wakiamua kusema Yesu
fufua roho zetu tuwe viumbe wapya tutoke katika makaburi, wote wanaweza
kufufuka na polisi wakakosa kazi,” alisema.
Askofu
Gamanywa pia aliwashutumu baadhi ya viongozi wa dini kwa madai kuwa
wamesahau wajibu wao na kufanya kazi ambazo hawajatumwa na Mungu.
“Sisi
viongozi wa roho na hapa nawazungumzia wakristo, tunatarajiwa kuleta
ufufuo wa roho za watu waliokufa, lakini tunafanya kazi nyingine ambazo
hatujatumwa na Mungu.
“Matamko
ya kukemea na kulaani ni staili ya wanasiasa, sisi tunayo mamlaka
inatoka juu. Hivyo basi, maneno yetu yanatakiwa kuwa ni habari za ufufuo
kwa wenye dhambi ambazo mamlaka za kawaida haziwezi kufanya bali Yesu
pekee.
“Tukihubiri watu wakaacha maovu, watafanya kazi bila kusukumwa, wataacha kazi haramu na wataacha uvivu.
“Kama
viongozi wa dini watashindwa kuwahubiria watu wakaacha kutenda maovu,
basi kazi hiyo itakuwa imewashinda na itabidi wajiuzuru.
“Kama
wewe ni mchungaji ama askofu halafu kuna watu wanaokufuata ibadani
lakini bado ni waongo, wezi, wafitinishaji, ujue kazi imekushinda.
“Kabla
hatujawaambia wanasiasa wajiuzuru, tunatakiwa tuanze sisi. Mimi
natangaza sijiuzuru bali nitawaambia ukweli, kwamba Yesu Kristo
amefufuka ni lazima umkubali na kumwamini ili ufufuke roho.
“We
must speak the truth (lazima tuseme ukweli), hata kama kuna watu wana
fedha nyingi na wanatoa sadaka kubwa ni lazima waambiwe ukweli,” alisema Askofu Gamanywa.
Askofu Mkuu KKKT
Mkuu
wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Fredrick
Shoo, alisema matukio ya utekaji yanajenga hofu ya kutoaminiana ambayo
si nzuri na ni hatari kwa nchi.
“Mambo
haya yanahitaji uthibitishisho, hivyo ni vema uchunguzi ufanyike na
ikithibitika hatua zichukuliwe kwa sababu yanazidi kuwatia hofu watu,” alisema.
Askofu
wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa,
Blaston Gavile, alisema mauaji ya askari wanane yaliyotokea wiki
iliyopita mkoani Pwani, yanasikitisha na watu wanatakiwa wafunge kwa
ajili ya kuliombea taifa.
Akitoa
salamu za Pasaka katika Usharika wa Kanisa Kuu mkoani hapa, Askofu
Gavile alisema kazi ya wakristo si kulalamika bali ni kumgeukia Mungu na
kumuomba aliepushe Taifa dhidi ya matukio ya utekaji, mauaji na
mengine.
“Kazi
ya wakristo si kulalamika mtaani kama ilivyo kwa mataifa mengine bali
kazi yao kubwa ni kufunga na kuomba kwa ajili ya taifa.
“Tuendelee kuliombea taifa na Mkoa wa Iringa, tuseme Mungu yatosha kuendelea kusikia matukio ya ajabu ndani ya nchi yetu,” alisema Askofu Gavile.
Naye
Askofu mstaafu wa Dayosisi hiyo, Dk. Owdenburg Mdegella, aliwataka
Watanzania kuacha kupoteza muda kujadili mambo yasiyo ya msingi badala
yake wajikite kujenga nchi.
Askofu
mstaafu wa Kanisa la Pentekoste (FPCT) mkoani Singida, Dk. Paulo
Samweli, alitoa rai kwa madhehebu ya dini nchini, kuliombea taifa
liweze kuondokana na umwagikaji wa damu kwa Watanzania wasio na hatia
wakiwamo polisi.
Akihubiri
katika ibada ya Pasaka katika Kanisa la Pentekoste mkoani humo, Dk.
Paulo alisema mauaji ya polisi wanane Kibiti, Pwani hayavumiliki na kila
mtanzania anapaswa kuyakemea yasijirudie.
Dk. Paulo alisema jukumu la polisi ni kulinda Watanzania wa madhehebu yote na wasiokuwa na dini na mali zao.
“Tukianza
kuwaua kwa ukatili namna hii, nani atatulinda? Wewe ukimuua polisi
ujue wazi kuwa unajiua wewe mwenyewe bila ya kujijua.
“Unyama huu haukubaliki mbele ya Mungu na kwa Watanzania wote, tuungane kuukomesha.
“Watu wasipofanya maombi vitendo hivyo vinaweza kusambaa sehemu mbalimbali nchini na matokeo yake nchi haitakalika tena.
“Shughuli
za kumwabudu Mungu kwa uhuru mpana kama ilivyo hivi sasa zitakuwa ni
ngumu na kujiletea maendeleo nako kutakuwa ni shida kutokana na kuwapo
viasharia vya uvunjifu wa amani,” alisema Askofu Dk. Paulo.

No comments