Ufafanuzi Juu Ya “Uzushi” Ulioenea Kwenye Mitandao Ya Kijamii Kuhusu Kufukuzwa Nchini Raia Wa Kenya, Wilayani Longido, Mkoa Wa Arusha.
Kumekuwepo
taarifa ambazo zimekuwa zikiripotiwa kupitia Vyombo mbalimbali vya
Habari pamoja na mitandao ya kijamii kuwa, Serikali ya Tanzania inafanya operesheni maalum inayolenga kuwaondoa Raia wa Kenya wanaoishi nchini bila kuwa na Vibali halali huko Wilayani Longido, Mkoa wa Arusha, huku wakimhusisha Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu katika utekelezaji wa ‘zoezi’ hilo.
Taarifa hizi zimezua tafrani na kutishia hali ya usalama iliyopo katika mpaka wa Tanzania na Kenya, Namanga.Tunapenda kutoa ufafanuzi kuhusu Taarifa hizo zinazoendelea kuenezwa kuwa:-
1.Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haijafanya operesheni yoyote inayolenga kuwakamata na kuwaondoa nchini raia wa Kenya
au Taifa lolote lile wanaoishi katika Wilaya ya Longido Mkoani Arusha
kama inavyoenezewa kwenye Vyombo vya Habari na Mitandao mbalimbali ya
kijamii.
2.Shughuli
za udhibiti wa raia wa kigeni wanaokiuka Sheria za Uhamiaji nchini
hazifanywi kwa kulenga Taifa lolote lile, bali hufanywa kwa kufuata
Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi. Wahusika wanaokiuka Sheria, Kanuni
na Taratibu za uhamiaji hukamatwa na kuchukuliwa hatua kwa makosa yao
binafsi na sio kwa msingi wa utaifa wao.
3.Kukamatwa kwa raia wa kigeni ambao walibainika kuwa ni raia wa Kenya
ni sehemu ya shughuli za kawaida za Idara ya Uhamiaji kama Chombo cha
Ulinzi na Usalama katika kuhakikisha kwamba raia wa kigeni wanatambuliwa
na kuishi kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi.
4.Suala la kukamatwa kwa raia hao wa Kenya ambao walibainika kukiuka Sheria ya Uhamiaji nchini halihusiani kwa njia yoyote ile na Serikali ya Tanzania kulenga kuwakamata raia wa nchi yoyote na wala si agizo la Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kama ilivyoripotiwa, bali ni utaratibu wa kawaida ambao unafanywa na
nchi yoyote katika kuhakikisha kwamba ukaazi wa wageni unazingatia
Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi husika. Kwa mfano, katika mwezi
Februari 2017, Idara ya Uhamiaji imewakamata wageni 396 kutoka mataifa
mbalimbali kwa makosa ya kiuhamiaji na kuwachukulia hatua mbalimbali kwa
mujibu wa Sheria.
5.Tanzania na Kenya
tunao uhusiano mzuri sana ambao ni wa kihistoria na nchi hii ni
mwanachama mwenzetu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa uhusiano huo,
wapo watanzania wengi wanaokwenda nchini Kenya kwa sababu mbalimbali kama vile matembezi, biashara, masomo nk. Pia wapo raia wengi wa Kenya wanaoingia na kuishi hapa nchini kwa sababu kama hizo hizo na hatuna tatizo nao, alimradi hawavunji Sheria za nchi yetu.
6.Mwisho,
tunatoa wito kwa Wageni wote wanaoishi hapa nchini kwa shughuli
mbalimbali kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za uhamiaji nchini. Wapo
baadhi ya wageni wanaoingia nchini kihalali, lakini wanaendelea kuishi
nchini hata baada ya muda waliopewa kuishi nchini kumalizika. Aidha,
wapo baadhi ya wageni wengine wanaoingia nchini kinyume cha sheria na
kuendelea kuishi nchini kinyume cha Sheria. Wale wanaobainika kukiuka
Sheria, Kanuni na taratibu za uhamiaji nchini watachukuliwa hatua kwa
mujibu wa sheria bila kujali utaifa wao.
7.Taarifa zinazoenezwa kupitia Vyombo vya Habari na Mitandao ya kijamii kwamba Tanzania inawalenga raia wa Kenya,
kuwakamata na kuwaondoa nchini si sahihi na zipuuzwe kwani zinalenga
kuchafua na kuzorotesha uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi zetu mbili
na wananchi wake, pamoja na kudhoofisha shughuli za udhibiti wa
wahamiaji haramu nchini.
8.Tunafahamu kuwa Tanzania
haiwezi kuishi kama kisiwa. Hivyo, tutaendeleza na kuimarisha
ushirikiano na Mataifa mengine pamoja na kuendelea kuweka mazingira
mazuri kwa wageni kuja na kuishi nchini kwa shughuli mbalimbali,
zikiwemo biashara, uwekezaji, utalii, matembezi na nyinginezo.
Imetolewa na;
KITENGO CHA UHUSIANO,
MAKAO MAKUU, IDARA YA UHAMIAJI,
BARABARA YA LOLIONDO, KURASINI,
S.L.P 512, DAR ES SALAAM.
31 MACHI, 2017.
www.immigration.go.tz

No comments