Korea Kaskazini Yatoa Vitisho Vingine kwa Marekani
Wakati
kukiwa na taharuki kati ya Marekani na Korea Kaskazini kuhusu matumizi
na majaribio ya mabomu ya nyuklia yanayofanywa na nchi hiyo ya bara la
Asia, imetoa msisitizo wa vitisho vingine.
Makamu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini, Han Song-ryol ameiambia BBC
kuwa nchi hiyo haiogopi vitisho vya Marekani na kwamba wamejipanga
kufanya majaribio ya makombora yake kwa mfumo wa kila wiki, kila mwezi
na kila mwaka.
Alisisitiza kuwa vita kamili ya nchi hiyo itakuwa ni matokeo ya Marekani kuchukua hatua zozote za kijeshi dhidi yake.
“Kama
Marekani inapanga mashambulizi ya kijeshi dhidi yetu, tutajibu kwa
makombora ya nyuklia kwa namna yetu na njia yetu wenyewe,” Han anakaririwa na BBC.
Kauli
hiyo imekuja ikiwa ni siku chache tangu Makamu wa Rais wa Marekani,
Mike Pence kuionya Korea Kaskazini kuwa muda wa kuivumilia umekwisha na
kuwataka waache kuijaribu Marekani.
Pence
alisema kuwa Korea Kaskazini haipaswi kumjaribu Rais Donald Trump
akiwataka kuona mfano wa kipigo alichowashushia Syria na Afghanistan
hivi karibuni.
Korea
Kaskazini imeendelea na mpango wake wa kuandaa na kufanya majaribio ya
mabomu ya nyuklia ingawa hatua hizo zimekuwa zikilaaniwa vikali na Umoja
wa Mataifa.
Nchi
hiyo imelenga katika kuhakikisha inatengeneza makombora yanayoweza
kufika katika pande kadhaa za dunia ikiwa ni pamoja na Marekani.
Rais
wa Marekani, Donald Trump amesema kuwa mpango huo hautawezekana na
tayari ameanza kutuma vikosi vya Marekani na Manuari za kivita katika
ufukwe wa Korea.

No comments