Bungeni: Serikali Yafuta Tozo Za Mazao Ya Chai, Pamba Na Kahawa- Majaliwa
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imefuta baadhi ya tozo katika
mazao ya pamba, chai na kahawa ambazo ni kero kwa wakulima ikiwemo ya
sh. 450,000 iliyokuwa inatolewa na kila kiwanda cha kuchambua pamba kwa
ajili ya kuchangia mbio za Mwenge.
Amesema
tozo nyingine iliyofutwa kwa zao la pamba ni ada ya vikao vya
Halmashauri za Wilaya ambayo ni sh. 250,000, ambapo katika zao la chai
kodi ya moto na uokoaji imeondolewa na kwenye zao la kahawa, ada ya
leseni ya kusindika kahawa ya Dola za Marekani 250 imefutwa.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Aprili 6, 2017) katika hotuba
yake ya mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato
na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka
2017/2018 Bungeni mjini Dodoma.
Amesema
kufutwa kwa tozo hizo ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali kwa wakulima
nchini ili kuwapunguza kodi, tozo na ada mbalimbali zinazochangia
kuwapunguzia faida.
“Serikali
pia imeboresha mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kuanzisha utaratibu wa
wazi wa ununuzi wa mazao kupitia minada na katika msimu wa mwaka
2016/2017 kwenye zao la korosho, utaratibu huo umechangia kwa kiasi
kikubwa kuongezeka kwa bei ya korosho kwa kilo kutoka sh 1,200 hadi sh
3,800, bei ambayo haijawahi kufikiwa katika historia ya zao la korosho
nchini,” amesema.
Amesema
mfumo huo wa stakabadhi ghalani na utaratibu wa minada umeongeza
ushindani na kuvutia wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi hususan
nchi ya Vietnam na nchi nyingine kuja wenyewe kununua korosho badala ya
kutegemea soko la India pekee.
Waziri
Mkuu amesema katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea na uchambuzi
wa kina wa kodi, tozo na ada zilizobaki katika sekta za kilimo, mifugo
na uvuvi kwa lengo la kuziondoa au kuzipunguza ili kumwezesha mkulima
kunufaika zaidi na jasho lake na kuongeza mapato ya Halmashauri.
Katika
hatua nyingine Waziri Mkuu amesema Bunge lilipitisha Sheria ya Huduma
za Habari Na. 12 ya mwaka 2016, ambayo ni muhimu katika kuimarisha
usimamizi na uwajibikaji katika Sekta ya Habari nchini, ambapo Kanuni za
Sheria hiyo zimeandaliwa na tayari zimeanza kutumika.
“Natoa
wito kwa wadau wa sekta ya habari kuzingatia sheria na kanuni hizo ili
kuimarisha weledi katika tasnia ya habari. Aidha, nashauri wadau wa
habari kujikita zaidi katika kuandika na kutangaza habari za masuala ya
maendeleo na uchumi ili kuwasaidia wananchi kutekeleza azma ya Serikali
ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda na kuboresha huduma za
kijamii,” amesema.
Pia
Waziri Mkuu amevikumbusha vituo vya televisheni kuweka wakalimani wa
lugha katika vituo vyao. Amesema katika mwaka 2017/2018, Serikali
itaendelea kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kutoa
vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye ulemavu shuleni na vifaa vya
kufundishia.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amesema kwamba Serikali imeendelea kutoa huduma
pamoja na kuongeza upatikanaji wa haki na fursa kwa watu wenye ulemavu
na katika kutimiza azma hiyo, amewaagiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kuwa
Kamati za Watu wenye Ulemavu zinaanzishwa katika ngazi za Mikoa,
Wilaya, Mitaa na Vijiji.
Pia
Serikali imeanzisha kampeni za kupinga unyanyapaa na vitendo vya
kikatili dhidi ya watu wenye ualbino katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza,
Geita, Simiyu, Kagera, Tabora, Kigoma, Mara, Mbeya, Katavi na Rukwa na
kampeni hiyo itaendelea nchi nzima.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S.L.P 980, DODOMA
ALHAMISI, APRILI 6, 2017.
No comments