Taarifa Toka IKULU: Rais Magufuli Akutana na Kufanya Mazungumzo na Balozi wa EU, Roeland Van de Geer na Balozi wa Israel, Yahel Vilan.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 06 Aprili, 2017 amefanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya
hapa nchini Mhe. Roeland Van de Geer na kuushukuru umoja wa nchi hizo
kwa kutoa msaada wa Euro Milioni 205 sawa na takribani Shilingi Bilioni
500 kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za maendeleo hapa nchini kwa
kipindi cha miaka 4 kuanzia mwaka huu.
Mhe.
Rais Magufuli amesema kutolewa kwa fedha hizo kumethibitisha uhusiano
na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya na kwamba
pamoja na kutoa fedha hizo umoja huo unatarajia kutoa fedha nyingine
kiasi cha Euro Bilioni 1.2 kwa ajili ya kuendeleza viwanda, kilimo na
uzalishaji wa nishati.
“Nimefurahi
sana kwamba uhusiano na ushirikiano wetu unajikita kushughulikia mambo
ya msingi kwa Watanzania, nakuhakikishia kuwa fedha mnazotoa zitatumika
vizuri na zitatoa mchango mkubwa katika maendeleo yetu” amesema Mhe.
Dkt. Magufuli.
Nae
Mhe. Balozi Roeland Van de Geer amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa
uongozi wake mzuri na dhamira yake ya kujenga uchumi na kusimamia
utawala bora ikiwemo mapambano dhidi ya rushwa, na pia amemuahidi kuwa
nchi wanachama wa umoja huo zitaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano
wake na Tanzania.
Wakati
huo huo, Mhe. Rais Magufuli amefanya mazungumzo na Balozi wa Israel
hapa nchini Mhe. Yahel Vilan na kumhakikishia kuwa Tanzania imedhamiria
kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Israel
hususani katika masuala ya uwekezaji, biashara, utalii na uboreshaji wa
huduma za kijamii.
Mhe.
Rais Magufuli amesema ili kufanikisha dhamira hiyo Tanzania imefungua
ubalozi nchini Israel na amemuomba Mhe. Yahel Vilan kupeleka ujumbe kwa
Waziri Mkuu wa Israel Mhe. Benjamin Netanyahu kuwa Tanzania itafurahi
kuona Israel inafungua ubalozi wake hapa nchini.
“Naamini
uhusiano na ushirikiano wetu utaongeza manufaa zaidi kwa nchi zetu na
watu wake, nimefurahishwa sana na taarifa kuwa watalii wataanza kuja kwa
ndege moja kwa moja kutoka Tel Aviv Israel na hivi karibuni ndege yenye
watalii zaidi ya 200 itakuja nchini kwetu, nawakaribisha sana watalii
na wawekezaji kutoka Israel” amesema Rais Magufuli.
Kwa
upande wake Mhe. Balozi Yahel Vilan pamoja na ujumbe wake amemueleza
Mhe. Rais Magufuli kuwa wamefurahishwa na ziara waliyoifanya hapa nchini
iliyowawezesha kukutana na viongozi mbalimbali na ameahidi kuwa
Serikali ya Israel itajenga jengo la wagonjwa mahututi (ICU) katika
Hospitali ya Benjamin Mkapa Mkoani Dodoma kuanzia mwishoni mwa mwaka
huu.
Mhe.
Balozi Yahel Vilan amemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa Israel
itaendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania kwa kuunga mkono juhudi
mbalimbali za maendeleo ikiwemo ujenzi wa viwanda, kilimo na kuimarisha
huduma za matibabu kwa wananchi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasilino ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Aprili, 2017
No comments