Mabweni Mapya ya UDSM Yaliyozinduliwa na Rais Magufuli Yatachukua Wanafunzi 3,840
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli, Jumamosi hii
amefanya uzinduzi wa mabweni mapya ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es
Salaam, UDSM.
Rais
Magufuli amesema kukamilika kwa mabweni hayo ya kisasa ndani ya kipindi
chini ya miezi minane ni ishara kuwa Tanzania inaweza. “Tukiamua
tunaweza tukafanya watu wakaona miujiza,” amesema.
Ameongeza
kuwa wapo watu walibeza kuwa shilingi bilioni 10 zisingeweza
kukamilisha ujenzi huo na kwamba hawakumiani kuwa yasingeweza kujengwa
na Watanzania. Ameshauri kuwa mafanikio hayo yawe vifundisho kwa
viongozi wa serikali kutotoa tenda kwa wakandarasi wa nje zenye gharama
kubwa na kuwaacha wale wa ndani.
Kwa
upande mwingine Rais amesema mabweni hayo yatalipiwa kwa shilingi 500
pekee, tofauti na 800 kwa mabweni mengine. Mabweni hayo yana uwezo wa
kuchukua wanafunzi 3,840.
Awali
akizungumza kwenye uzinduzi huo, makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa
Rwekaza Mukandala alissema mabweni hayo yana vitanda 1,920 vya double
decker, makabati 1,920, shelves za vitabu 1,920, meza, 1,920, viti 3,840
magodoro 3,840.
“Tutahakikisha
kuwa huduma zote muhimu kama vile cafeteria ya chakula, maduka kwaajili
ya mahitaji mbalimbali, zahanati, salon, kituo cha polisi na nyinginezo
vinapatikana hapa hapa,” alisema Profesa Mukandala.
Aliongeza
kuwa ujenzi wa cafeteria umeshaanza na ikikamilika itakuwa na uwezo wa
kuchukua wanafunzi 500 kwa wakati mmoja. Amehakikisha kuwa chuo
kimejipanga kuhakikisha kuwa mabweni yanatunzwa na tayari wameshampata
msimamizi mkuu aliyepewa mafunzo maalum ya muda mfupi.
Prof
Mukandala alimshukuru Rais Magufuli kwa namna alivyojitolea kuhakikisha
mabweni hayo yanakamilika kwa kufuatilia kwa ukaribu kila hatua za
ujenzi wake.
“Hili ni jambo kubwa sana na historia itaandikwa kwa herufi za dhahabu,” alisema.
Aliongeza
kuwa wizara tatu zimehusika kwenye ujenzi wa mabweni hayo ambazo ni
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga taifa, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Mawaziri wote
wa wizara hizo Dr. Hussen Mwinyi, Profesa Makame Mbarawa na Profesa
Joyce Ndalichako walikuwepo.

No comments