SHIRIKA
la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limekiri mbele ya Kamati ya Bunge
ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwa linaweza kupoteza kiasi cha Sh bilioni
270, zilizoingizwa kwenye mradi wa ubia baina yake na Kampuni ya Azimio
Housing Estates (AHEL), kama shirika hilo lisipokuwa makini.
Pamoja na hayo, kamati hiyo baada ya
kubaini madudu kadhaa katika hesabu za shirika hilo, imemuagiza Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi maalumu wa
mikopo yote iliyotolewa na NSSF kwa vyama vya akiba na mikopo.Akijibu
hoja za wajumbe wa kamati hiyo kuhusu mradi huo ambao ni ujenzi wa mji
wa kisasa katika eneo la Dege Kigamboni jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi
Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara alisema kwa sasa kinachoangaliwa
kwenye mkataba huo ni athari za kupoteza fedha hizo.
Profesa Kahyarara alisema pamoja na
shirika hilo kuwepo kwenye ubia huo, lakini limegundua ekari zilizopo
kwenye mkataba si za uhalisia.
Alisema kwa mujibu wa mkataba
zilitakiwa ziwe ekari 20,000 lakini kiuhalisia baada ya kufanya tathmini
zipo ekari zaidi ya 3,500.
Aidha, alifafanua kuwa bei
iliyothaminiwa kwenye ekari hizo pia ni tofauti kwani mwekezaji huyo
alithaminisha ardhi hiyo kwa Sh milioni 800, lakini baada ya NSSF
kufanya uchunguzi wake ikabaini kuwa ekari moja thamani yake ni Sh
milioni 25.
Kwa mujibu wa taarifa za CAG zinaeleza
kuwa NSSF iliingia ubia na kampuni hiyo na kuanzisha kampuni maalumu kwa
jina la Hifadhi Builders Limited.
Katika mkataba huo, Azimio Housing
Estates itatakiwa kuendeleza ekari 20,000 za ardhi zilizopo Kigamboni
kwa ajili ya ujenzi wa mji mpya wa kisasa wa Kigamboni kupitia mradi
uliopo eneo la Dege.
Hata hivyo, mradi huo umesimama
utekelezaji wake tangu Februari, mwaka huu kutokana na mwekezaji
kutokuwa na fedha huku NSSF tayari ikiwa imeshaingiza Sh bilioni 270.
Katika ubia huo, NSSF inamiliki
asilimia 45 ya hisa wakati Azimio Housing Estates inamiliki asilimia 55
ya hisa na jumla ya gharama za mradi ni Dola za Marekani milioni 653.44.
No comments