Mwanza: RC John Mongella akumbana na vilio vya njaa Sumve
Wakazi
zaidi ya 300 wa Kata ya Mwagi wakiongozwa na mbunge wao wa Sumve,
Richard Ndassa wamepokea msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John
Mongella kwa mabua ya mahindi mikononi mwao, kuashiria namna zao hilo
lilivyoathiriwa na ukame.
Mongella
ambaye alikuwa ameambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya
hiyo, wakati wa ziara yake kukagua maendeleo ya kilimo wilayani hapa,
alikutana na hali hiyo katika Kijiji cha Mwabilanda wakati akitokea
Kijiji cha Manawa kukagua mashamba ya pamba.
Wakazi hao walisema wametekeleza wajibu wao, lakini ukame umevuruga malengo yao huku wakiomba msaada wapelekewe chakula haraka.
Awali,
akiwa Kijiji cha Manawa wakazi wake walisimama barabarani kwa lengo la
kutaka wapatiwe ufumbuzi wa namna Serikali ilivyojipanga kuwanusuru na
njaa iliyosababishwa na ukame.
“Kwa
kweli hali yetu ya chakula hapa kijijini ni mbaya. Mimi na umri wangu
sijawahi kushuhudia hali kama hii kwa zaidi ya miaka 40,” alisema mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho, Joseph Nkonoki.
Alifafanua
kuwa baadhi ya wanaume wameanza kutelekeza familia zao kutokana na
kukosa namna ya kupata fedha kwa ajili ya kununua chakula.
Akijibu malalamiko hayo Mongella alisema: “Timu
ya mkoa itakutana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya wiki ijayo
ili kuandaa taarifa ambayo baadaye Serikali itaifanyia kazi.Matokeo yake
mtayaona muda siyo mrefu.”
Mongella aliwashauri wakazi hao kulima mazao yanayostahimili ukame katika kipindi hiki ambacho mvua zimekuwa za kusuasua.
Aliwataka kuwa na subira wakati Serikali ikiendelea kujipanga, huku akisema ukame unachangiwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Pia,
Mongella alimuagiza mkuu wa wilaya hiyo, Mtemi Simeon kuwakamata na
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wananchi watakaobainika kukata miti
bila kibali chake.

No comments