Waziri wa Ujenzi Prof. Mbarawa atoa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi Mkuu wa ATCL kufanya mabadiliko ya menejimenti ya Shirika hilo
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ametoa muda
wa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL),
kufanya mabadiliko katika menejimenti ya Shirika hilo ili kuongeza
ufanisi na kuboresha utendaji kazi.
Ametoa
agizo hilo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza katika mkutano wa
Menejimenti pamoja na wafanyakazi wa Shirika hilo na kuwataka kutoa
huduma bora ili kulifanya Shirika hilo kuwa miongoni mwa mashirika bora
ya ndege barani Afrika.
“Nataka
ndani ya mwezi mmoja uwe umeshafanya mabadiliko katika menejimenti,
mabadiliko lazima yaanzie juu kwanza kwa watoa maamuzi na ishuke hadi
kwa wafanyakazi wazembe na wasio waadilifu,” amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Waziri
Mbarawa amepinga nyongeza ya mshahara kwa wafanyakazi wa Shirika hilo
hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali ipo katika juhudi za kulifufua
na kuliimarisha Shirika hilo.
Aidha
Waziri Mbarawa ameitaka Idara ya Masoko ya shirika hilo kuzunguka
katika taasisi zote zilizo chini ya Wizara yake na kuzishawishi kuweza
kutumia huduma za usafiri wa anga wa ATCL.
“Serikali imekamilisha upande wake wa ununuzi wa ndege, sasa kazi inabaki kwenu, sitaki watu wa masoko kukaa ofisini”, amesema Prof. Mbarawa.
Ameongeza
kuwa wafanyakazi wa ATC wanatakiwa kujipanga kutoa huduma iliyotukuka
kwa wateja wake ili kuweza kuhimili ushindani uliopo katika mashirika ya
ndege nchini.
“Inabidi
tofauti kubwa ionekane kati yenu na mashirika mengine, yeyote ambaye
anaona hawezi kutoa huduma bora kwa mteja atafute sehemu nyingine kwani
hapa hatufai ”, amesisitiza Waziri Mbarawa.
Profesa
Mbarawa amelitaka shirika hilo kutumia mfumo wa kisasa wa kukata tiketi
kwa njia ya simu na kompyuta ili kuwarahishia watumiaji wa shirika hilo
kuweza kupata tiketi kwa haraka na urahisi.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Eng. Ladislaus Matindi
amemhakikishia Waziri Mbarawa kufanyia kazi maagizo aliyotoa na kuahidi
kuboresha utendaji kazi wa shirika hilo kwa lengo la kuteka soko la
ushindani wa usafiri wa anga nchini.
“Kwa
sasa tumeanza vizuri na naamini uwezo wa kuzalisha faida zaidi tunao,
tunaahidi kuboresha utendaji kazi ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya
Serikali ya Awamu ya Tano,” amesema Eng. Matindi.

No comments