• Breaking News

    Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Aongoza Wabunge Kuaga Mwili Wa Mbunge Wa Dimani- Hafid Hally Tahir

    WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameongoza wabunge kuuaga mwili wa aliyekuwa mbunge wa Dimani, Zanzibar Mheshimiwa Hafidh Ally Tahir.

    Bw. Tahir amefariki saa 9 alfajiri ya kuamkia leo katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na mwili wake kuagwa katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma kabla ya kusafirishwa kwenda Zanzibar kwa mazishi.

    Akizungumza katika tukio hilo, Waziri Mkuu ametoa pole kwa Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai, familia ya marehemu na wabunge wote.“Tumepokea taarifa za msiba huu kwa mshtuko mkubwa. Leo tupo katika wakati mgumu sana. Tumeondokewa na viongozi wengi,” amesema.

    Amesema wafiwa wanatakiwa kuishi kwa upendo. “Tumuombee marehemu, tuiombee familia iwe na moyo wa utulivu katika kipindi kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao.”

    Bw. Hafidh alizaliwa Oktoba 30, 1953 na aliwahi kuwa Mkuu wa Sauti ya Tanzania Zanzibar (1970-1978) na amekuwa mbunge tangu 2005 hadi mauti yanamkuta.Enzi ya uhai wake, alishiriki kikamilifu katika masuala ya michezo; alikuwa mwamuzi wa soka mwenye beji ya FIFA na kocha msaidiizi wa timu ya soka ya Bunge.

    Hadi jana, Bw. Hafidh alishiriki katika shughuli mbalimbali ikiwemo uchaguzi wa kupata viongozi wa Tawi la Umoja wa Wabunge WanaYanga mjini Dodoma ambapo yeye alichaguliwa kuwa Katibu.

    IMETOLEWA NA:
    OFISI YA WAZIRI MKUU,
    S. L. P. 980,
    DODOMA.
    IJUMAA, NOVEMBA 11, 2016.

    No comments

    Post Top Ad