WATU
wanne wakiwemo raia watatu wa Burundi, wanashikiliwa na Polisi mkoani
Morogoro baada ya kukutwa na magamba ya kakakuona, yenye thamani ya
zaidi ya Sh bilioni 1.4.
Walikuwa wamehifadhi magamba hayo
kwenye mifuko 67, yakisubiri kusafirishwa kwenda nje ya nchi kuuzwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei, alisema watu hao
walikamatwa saa tano na nusu usiku wa Oktoba 28, mwaka huu eneo la mtaa
wa Reli, kata ya Kichangani, Manispaa ya Morogoro.Walinaswa ndani ya ghala moja, lenye mashine ya kukoboa na kusaga nafaka.
Alisema, askari wa jeshi hilo wakiwa
katika msako, walipokea taarifa za kiintelejensia kutoka kwa raia wema
kuhusu mazingira ya watu katika eneo hilo. Walipofika, walikuta
watuhumiwa hao wanne.
Baada ya upekuzi kwenye ghala hilo,
polisi walikamata magamba ya kakakuona katika mifuko 67, baaadhi yake
yakiwa tayari kwa ajili ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi.
Kamanda Matei aliwataja raia wa Burundi
waliokamatwa kuwa ni Kibonese Golagoza ( 35), Nuru Athuman (32) na
Benjamin Gregory Luvunduka (41) ambao pia ni wakazi wa Morogoro, wakati
Mtanzania ni Shukuru Mwakalebela (25) mkazi wa Stesheni mjini hapa.
Alisema magamba hayo, yalifungwa katika
mifuko yenye kilo 50 na kisha kutumbukizwa kwenye viroba vikubwa vya
kilo 100, vilivyochanganywa na maharage. Aidha alisema watuhumiwa raia
wa Burundi, wanakabiliwa pia na tuhuma za kuingia nchini bila kibali cha
Uhamiaji.
Ofisa Maliasili wa Mkoa wa Morogoro,
Joseph Chuwa aliyekuwepo katika upekuzi huo, alisema katika mifuko 67
iliyokamatwa, kila mmoja ulikuwa na wastani wa magamba ya kakakuona
1,000.
Alisema kakakuona mmoja, kwa wastani
anakuwa na magamba 60 hadi 100, hatua iliyofanya kila mfuko kuwa na
wastani wa kakakuona wapatao 10 waliouawa kwa ajili ya biashara hiyo
haramu.
Alisema kutokana na idadi ya mifuko
hiyo, wastani wa kakakuona 670 waliuawa, ambapo kilo moja ya magamba
yake huuzwa kwa dola za Marekani 960, hivyo kutokana na viwango vya sasa
vya thamani ya dola kwa fedha ya Tanzania, ni sawa na Sh bilioni 1.4.
No comments