HESLB yafafanua vigezo utoaji mikopo, Waliokosa sababu zatajwa, wapewa nafasi ya kukata rufaa
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo Bw. Abdul-Razaq Badru akifafanua
jambo katika mkutano na wanahabari jijini Dar es Salaam leo (Jumapili,
Oktoba 30, 2016). Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na
Mawasiliano wa Bodi hiyo Bw. Cosmas Mwaisobwa.
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa ufafanuzi
kuhusu vigezo inavyotumia katika kuchambua, kupanga na kutoa mikopo kwa
wanafunzi 20,183 (asilimia 74) wa mwaka wa kwanza hadi sasa kati ya
25,717 iliyopanga kuwapa mikopo katika mwaka huu wa masomo, 2016/2017.
Idadi iliyobaki (asilimia 26) ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza itajazwa
na waombaji ambao baadhi ya nyaraka walizowasilisha zinaendelea
kuchambuliwa ili kuthibitisha uhalisi wake na baadhi zitajazwa na
waombaji ambao wanakata rufaa na kuwasilisha nyaraka zinazothibitisha
uhitaji wao kwa mujibu wa vigezo vya mwaka huu.
Aidha, katika mwaka huu wa masomo, Serikali imepanga kutumia jumla ya
Tshs 483 kutoa mikopo kwa wanafunzi 93,295 wanaoendelea na 25,717 wa
mwaka wa kwanza.
Katika mkutano na waandishi wa habari leo (Jumapili, Oktoba 30, 2016),
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru amesema vigezo vikuu
vinavyotumika mwongozo uliotangazwa na Bodi hiyo wakati ilipotangaza
kuanza kupokea maombi mwezi Juni mwaka huu ambao unataja makundi makuu
matatu ya watakaopata mikopo.
Vigezo vilivyotumika kutoa mikopo
Kwa mujibu wa Bw. Badru, kundi la kwanza linajumuisha wanafunzi waombaji
wa mikopo wenye uhitaji maalum kama wenye ulemavu uliothibitishwa na
Waganga Wakuu wa Wilaya na yatima ambao katika maombi yao waliwasilisha
nakala za vyeti vya vifo zilizothibitishwa na makamishna wa viapo.
“Kundi la pili linajumuisha waombaji wa mikopo ambao baada ya uchambuzi
wa taarifa zao walizowasilisha na baada ya kulinganisha na gharama za
jumla za masomo yao ya sekondari, wamebainika kuwa wana uwezo mdogo wa
kugharamia masomo yao ya elimu ya juu na hivyo kuwa na uhitaji zaidi wa
mikopo,” amesema Bw. Badru.
Katika mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari
(MAELEZO), Bw. Badru ametaja kundi la tatu na la mwisho kuwa
linajumuisha waombaji wa mikopo ambao wenye ufaulu wa juu katika matokeo
yao ya kidato cha sita na wamechaguliwa kujiunga na fani za kipaumbele
kwa taifa.
Fani hizo ni Sayansi za Tiba, Ualimu wa Sayansi na Hisabati, uhandisi wa
Kilimo, Mafuta na Gesi na Sayansi za Ardhi, Usanifu Majengo na
Miundombinu.
Makundi ya wanafunzi waliopata mikopo
“Hivyo basi, hadi sasa tumetoa mikopo kwa wanafunzi 20,183 wakiwemo
wanafunzi yatima 4,321, wenye ulemavu 118, wanafunzi wenye uhitaji
waliosomeshwa na taasisi mbalimbali katika masomo ya sekondari (87),
wanafunzi wanaosoma kozi za kipaumbele 6,159 na wanafunzi wanaosoma kozi
zisizo za kipaumbele lakini wanaotoka kwenye familia duni 9,498,”
amefafanua Bw. Badru.
Sababu za kukosa mikopo
Katika mkutano huo, kiongozi huyo wa HESLB pia ameeleza kwa kina sababu nyingine za waombaji 27,053 ambao hawajapangiwa mikopo.
Ametaja sababu hizo kuwa ni pamoja na baadhi ya waombaji (90) kuwa na
umri wa zaidi ya miaka 30, waombaji mikopo waliopata udahili kwa sifa
linganishi (equivalent qualifications) na waombaji waliomaliza masomo ya
kidato cha sita zaidi ya miaka mitatu iliyopita.
Kundi jingine la waombaji waliokosa mikopo katika awamu ya kwanza ni
waombaji waliopata nafasi katika vyuo kwa ufaulu wa mitihani waliyofanya
kama watahiniwa binafsi (Private Candidates) na waombaji ambao
hawakurekebisha fomu zao za maombi ingawa waliitwa kufanya hivyo.
Nafasi ya rufaa na uhakiki wa wanafunzi wanaoendelea na masomo
Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji huyo pia amewataka waombaji
ambao hawajaridhika na upangaji wa mikopo unaotangazwa, kuwasilisha
rufaa zao kwa njia ya mtandao utakaofunguliwa kuanzia katikati ya wiki
ijayo.
“Tunafahamu kuwa kuna baadhi ya wanafunzi wamekosa mkopo kwa
kutowasilisha baadhi ya nyaraka ingawa tuliwaomba kufanya hivyo, hawa na
wengine wenye sababu za msingi, watapata fursa ya kuwasilisha rufaa zao
kwa njia ya mtandao na nakala kuzituma kwa utaratibu tutakaoutangaza
wiki inayoanza kesho,” amesema Bw. Badru.
Aidha, katika mkutano huo, Bw. Badru amesema bodi ya Mikopo inatarajia
kuanza kazi kuhakiki taarifa za wanafunzi wanaoendelea na masomo ambao
wanapata mikopo ya elimu ya juu kwa lengo la kubaini kama ni wana
uhitaji wa mikopo hiyo kwa mujibu wa vigezo au hapana.
Katika zoezi hili linalotarajiwa kufanyika kwa siku 30 kuanzia mwezi
ujao (Novemba, 2016), wanafunzi wote ambao ni wanufaika watalazimika
kujaza dodoso maalum litakalokusanya tarifa za kiuchumi za wazazi na
walezi wao ili kuweza kupata uhalisia wa sasa.
“Wanafunzi watakutana na dodoso katika akaunti zao katika mtandao wetu
wa maombi ya mikopo (OLAMS) na watapaswa kujaza. Wale ambao hawatajaza
dodoso hili kwa njia ya mtandao tutasitisha mikopo yao na wale ambao
baada ya uchambuzi tutabaini hawana uhitaji, nao tutasitisha mikopo yao
na watapaswa kuanza kurejesha fedha walizokopokea,’ amefafanua.
HESLB ilianzishwa mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai mwaka 2005
kwa lengo la kutoa mikopo kwa watanzania wahitaji waliopata nafasi za
masomo katika vyuo vya elimu ya juu na kukusanya mikopo iliyoiva kutoka
kwa wadaiwa walionufaika na mikopo tangu mwaka 1994.
No comments