• Breaking News

    ATHARI ZA UGONJWA WA KISUKARI




    Kisukari ni mojawapo ya magonjwa ya mmeng’enyo ambayo husababisha kuwepo kwa kiwango kikubwa cha sukari katika damu kwa muda mrefu. Dalili kuu za ugonjwa huu ni kukojoa mara kwa mara isivyo kawaida, hususan nyakati za usiku, kuhisi kiu ya maji, mwili kuchoka, kupungua uzito wa mwili na misuli, kupata muwasho katika viungo vya uzazi, majeraha ya kujikata na kuumia yanayopona taratibu na kutokuona vizuri kwa sababu ya ukavu wa
    macho.

    Kuna aina tatu za ugonjwa huu nazo ni kisukari aina ya 1, kisukari aina ya 2, na kisukari wakati wa ujauzito.


    Kisukari aina ya 1 ni ugonjwa ambao mwili hautengenezi homoni ya insulini. Ugonjwa huu mtu huweza kuupata katika umri mdogo na pia mtu anaweza kuupata ugonjwa huu hadi anapofikia umri wa miaka arobaini. Ni asilimia ndogo ya idadi ya watu hupata ugonjwa huu wa kisukari aina ya 1.
    Wagonjwa wenye kisukari aina ya 1 wanahitajika kutumia aina ya insulini ya kuchoma kwa sindano kwa maisha yao yote. Na ni lazima wawe na utaratibu wa kupima kiwango cha sukari katika damu mara kwa mara pamoja na kuzingatia mlo maalum ili kuepuka kiwango cha juu cha sukari katika damu.


    Kisukari aina ya2 ni ugonjwa ambao mwili wa mgonjwa hautengenezi homoni ya insulini ya kutosha kwa ajili ya kurekebisha sukari, au seli za mwili za mgonjwa zinakuwa zimepungua au hazina hisia dhidi ya homoni ya insulini na kushindwa kuchukua sukari kutoka katika damu ili iweze kumeng,enywa na kutengeneza nishati au kuhifadhiwa mwilini (hujulikana pia kama usugu wa insulini). Kadirio la 90% ya wagonjwa wa kisukari wana aina hii ya ugonjwa.


    Baadhi ya watu wanaweza kumudu aina hii ya 2 ya kisukari kwa kupunguza uzito, kula mlo sahihi (healthy diet), kufanya mazoezi pamoja na upimaji wa kiwango cha sukari katika damu.Mbali na mazoezi na kuzingatia mlo sahihi, aina hii ya ugonjwa hutibiwa kwa kutumia dawa za vidonge vya kumeza ambavyo husaidia ufanyaji kazi wa homoni ya insulini. Aina ya pili ya kisukari isipotibiwa ugonjwa waweza kuendelea na kuwa sugu na hapo mgonjwa huitaji kupewa homoni ya insulini.


    Wale walio na uzito mkubwa au uzito mkubwa kupindukia(obesity), wako katika hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari aina ya 2 ukilinganisha na wale walio na uzito wa kawaida. Watu walio na mkusanyiko wa mafuta mwilini, mafuta katika tumbo (kitambi) wako katika hatari ya kupata ugonjwa.Kuwa na uzito mkubwa au uzito wa kupindukia husababisha mwili kutengeneza kemikali zinazoathiri mishipa ya damu na moyo, pia huathiri mfumo wa mmeng’enyo.


    Kuwa na uzito mkubwa,au kutoshiriki kazi za kuupa mwili mazoezi ya kutosha, pamoja na kula bila mpangilio kunaiweka miili yetu katika hatari ya kupata aina hii ya 2 ya kisukari. Mfano unywaji wa vinjwaji baridi vyenye sukari kama soda kila siku, unaongeza hatari hiyo. Wanasayansi wanaamini kuwa athari ya sukari katika vinywaji baridi yaweza kuwa ya moja kwa moja, zaidi ya kuongeza uzito wa mwili.


    Katika utafiti mmoja huko nchini Uingereza, ulionyesha kuwa wanaume wenye kiwango kidogo cha homoni ya testosterone walikuwa katika hatari ya kupata aina ya 2 ya kisukari.

    Aina ya 3 ni kisukari wakati wa ujauzito (kitaalam hujulikana kama gestational diabetes),ugonjwa huwaathiri wanawake wakati wa ujauzito.Katika kipindi cha ujauzito baadhi ya kinamama huwa na kiwango kikubwa cha sukari katika damu na kuifanya homoni ya insulini kushindwa kumudu sukari hiyo kuchukuliwa na seli za mwili na kupelekea kuendelea kuongezeka kwa kiwango cha sukari katika damu.


    Uchunguzi hufanyika wakati wa ujauzito, na wagonjwa wengi wa aina hii huweza kutibiwa kwa kufanya mazoezi pamoja na kuzingatia mlo sahihi. Asilimia ndogo ya wagonjwa ambao njia ya awali ya kutibu itashindikana, kiwango cha sukari hupunguzwa kwa kutumia dawa za vidonge za kumeza. Na endapo kisukari hakitagundulika au hakitatibiwa wakati wa ujauzito kutapelea matatizo wakati wa kujifungua.Mtoto anaweza kuwa mkubwa zaidi ya kawaida na kumsababishia mama matatizo.

    Watafiti waligundua kuwa, kina mama walao kiasi kikubwa cha mafuta yatokanayo wanyama na lehemu kabla ya ujauzito wanakuwa katika hatari ya kupata kisukari wakati wa ujauzito ukilinganisha na wakinama wanaokula kiwango kidogo cha mafuta ya wanyama na lehemu.


    Matibabu.
    Kisukari aina ya 1 ni aina ambayo mtu huishi na ugonjwa kwa maisha yote na mpaka sasa hakuna tiba inayojulikana kuondoa ugonjwa. Aina ya 2 ni ile ambayo huweza kudumu kwa maisha yote, lakini mgonjwa anaweza kuondokana na dalili za ugonjwa kwa kutumia dawa,mazoezi pamoja na mlo sahihi. Baadhi ya watu wameweza kumudu kuondokana na dalili za ugonjwa bila kutumia dawa kwa aina hii ya 2, na hii imewezekana kwa kutumia mazoezi,mlo sahihi na kudhibiti uzito wa mwili.

    Wagonjwa wenye aina ya kwanza ya kisukari hutibiwa kiwango cha sukari katika damu kwa kutumia homoni ya insulini kwa njia ya kuchoma sindano, pamoja na mlo sahihi na mazoezi. Wagonjwa wenye aina ya 2 pili hutibiwa kwa dawa za vidonge lakini wakati mwingine hata homoni ya insulini hutumika.


    Ni muhimu kiwango cha sukari katika damu kutokuwa juu isivyo kawaida ili kuepuka madhara kwa mgonjwa. Yafuatayo ni madhara awezayo pata mgonjwa endapo hatatibiwa kisukari.

    Matatizo ya moyo-kuziba kwa mishipa ya damu ya kwenye moyo na kupunguza mzunguko wa damu kwenye misuli ya moyo (ischemic heart diseases).
    Shinikizo la juu la damu-ni kawaida kwa watu wenye ugonjwa sugu wa kisukari na huweza kupelekea hatari ya kupata magonjwa ya figo,macho, shambulizi la moyo na kiharusi.
    Kuathirika afya ya akili-Ugonjwa wa kisukari usipotibiwa, mgonjwa anaweza kupata matatizo ya msongo wa mawaza,sononi , wasiwasi na hata magonjwa mengine ya akili.
    Magonjwa ya fizi-ugonjwa umekuwa ukiwashambulia zaidi wale wenye kisukari.
    Kupoteza uwezo wa kusikia.
    Magonjwa ya uambukizi ya ngozi.
    Matatizo ya miguu- vidonda visivyopona, miguu kuwaka moto(peripheral neuropathy).
    Matatizo ya macho.
    Matatizo ya tumbo.
    Mkusanyiko wa tindikali katika damu.
    Kuathirika kwa mishipa ya fahamu.
    Tatizo la nguvu za kiume.


    Katika nyakati hizi kuna ongezeko la wagonjwa wengi wanaougua maradhi ya kisukari ukilinganisha na miaka ya nyuma. Hii inachangiwa na kubadilika kwa mfumo wa maisha. Ni vyema basi kuhakikisha kuwa unaonana na wataalam wa afya mapema endapo utapata dalili za ugonjwa huu ili kuudhibiti na kuepuka madhara yatokanayo na ugonjwa wa kisukari.

    No comments

    Post Top Ad