Wapinzani Wadai Wakurugenzi Waliotumbuliwa wanalipwa Milioni 480 kwa mwezi
Maoni
ya upinzani ya wizara mbili, jana yaliibua hoja tofauti; ya kwanza
ikidai Serikali inawalipa wakurugenzi 120 waliotumbuliwa Sh480 milioni,
na ya pili ikikikishutumu kiti cha Spika kwa kuzuia mjadala wa wabunge
kutishiwa maisha.
Katika
sakata la kwanza, wapinzani walisema fedha za Serikali zinapotea
kutokana na watumishi waliotumbuliwa au kuachwa katika uteuzi kuendelea
kulipwa stahiki zao.
Msemaji
wa kambi hiyo, Japhary Michael alisema wakati akitoa maoni kuhusu
bajeti ya Tamisemi kuwa wakurugenzi hao wanalipwa mshahara wa Sh5.76
milioni kila mmoja kwa mwezi.
“Ikumbukwe
kuwa wakurugenzi hawa bado wanalipwa mishahara yao pamoja na stahiki
nyingine za kiutumishi kama nyumba, umeme, simu, matibabu na kadhalika.
Wastani wa mshahara wa mkurugenzi ni Sh 3.8 milioni mpaka Sh4 milioni,” alisema.
Alisema
wakurugenzi 120 wa zamani hawakuteuliwa kwa nafasi hizo katika Serikali
ya Awamu ya Tano lakini bado wamo katika utumishi wa umma, na hata wale
wapya walioteuliwa walitoka nje ya mfumo wa utumishi wa umma, wengi wao
wakiwa makada wa CCM.
Alisema
baada ya kutenguliwa kwa wakurugenzi hao 120 kutoka halmashauri
mbalimbali nchini, walielekezwa kuripoti kwa makatibu tawala wa mikoa
waliyotoka kwa ajili ya kupangiwa kazi nyingine.
“Ni
zaidi ya mwaka mmoja sasa wakurugenzi hawa takribani wote wanahudhuria
kwa makatibu tawala wa mikoa na kimsingi hawana kazi za kufanya,” alisema.
Alisema
kambi hiyo inaishauri Serikali kuangalia upya sheria ya utumishi na
ajira katika serikali za mitaa ili kuwe na utaratibu ambao mchakato wake
utaanzia katika vikao kisheria vya halmashauri.
Michael,
ambaye ni mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), alishauri Waziri ateue
kutokana na orodha itakayopendekezwa na halmashauri baada ya watu kuomba
ajira.
Katika
sakata la pili, msemaji wa kambi ya upinzani bungeni anayehusika na
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ruth
Mollel alidai kiti cha Spika kilizuia mjadala wa wabunge kutishiwa
maisha kwa mgongo wa kanuni za Bunge.
Suala
hilo lilimfanya waziri husika, Jenista Mhagama kusimama na kutaka
sentensi hiyo ifutwe kwa kuwa ilishaondolewa wakati kiongozi wa upinzani
bungeni, Freeman Mbowe alipokuwa akisoma maoni yao kuhusu bajeti ya
Ofisi ya Waziri Mkuu.
Lakini
hoja hiyo ilipingwa na mbunge wa Iringa, Mchungaji Peter Msigwa
aliyesema kuwa Katiba inawapa uhuru wa kusema maneno hayo.
Hata
hivyo, Spika Job Ndugai alisema maoni hayo yaliandikwa na mtu ambaye
haelewi taratibu za Bunge na hivyo kufuta sentensi hiyo.
Alihoji kama kuna mbunge aliyepeleka taarifa ya kutishiwa maisha.
Kuhusu hoja kwamba wapinzani wanadhibitiwa, Ndugai alihoji wanadhibitiwaje.
“Hivi
kwa nini mnajiweka katika hali fulani ya kuona kwamba mnaonewa? Hivi
unaonewa na nani kanuni ni za wote? Taratibu ni za wote hakuna mtu
aliyedhibitiwa chochote,” alisema.

No comments