Maalim Seif Amvaa Lipumba, Msajili wa Vyama..
Licha
ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kudai kuwa Baraza la
Uongozi la chama hicho limemvua madaraka Katibu Mkuu Maalim Seif
Sheriff Hamad kwa madai kwamba ameshindwa kutekeleza majukumu yake.
Maalim
Seif jana Aprili 9,2017 jijini Dar es Salaam aliibuka na kueleza hujuma
4 nzito alizodai zimetekelezwa na Lipumba kwa kushirikiana na vyombo
vya dola, kwa kutumia mgongo wake kukidhoofisha chama hicho, huku
akijinasibu kuwa hajashindwa kutekeleza majukumu yake na kuahidi kwamba
mara baada ya kumaliza ziara ya ujenzi wa chama Zanzibar atahamia Bara
ili kudhihirishia wanachama hajashindwa kufanya kazi.
Maalim
Seif alitangaza vita dhidi ya Profesa Lipumba na kundi lake huku
akisisitiza kuwa yeye bado Katibu Mkuu hadi pale atakaposimamishwa na
Baraza Kuu la Uongozi halali la chama hicho au kufukuzwa uanachama na
Mkutano Mkuu halali wa CUF.
“Tumevumilia
vya kutosha sasa basi, tutailinda CUF kwa gharama yoyote ile na nyie
mlio nyuma ya mgogoro huu mtabeba dhamana kwa mliyoyatenda. Hakuna tena
cha kunitisha na kunikatisha tamaa na tulipofika tutapata ushindi,” amesema.
==>Miongoni mwa hujuma 4 alizotaja Seif dhidi ya CUF, ni pamoja na;
1.Vyombo vya dola kumzuia kufanya shughuli za kisiasa upande wa Tanzania Bara
2.Lipumba kuvamia na kuteka baadhi ya ofisi za CUF
3.Wizi wa fedha za ruzuku
4.Bunge kupokea wagombea feki wa chama hicho katika uchaguzi wa Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
Licha
ya hayo, Maalim Seif ameitaka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini
(RITA) kutokubali kushiriki njama ovu aliyodai kuwa imelenga kusajili
wajumbe feki wa Bodi ya Wadhamini CUF kwa minajili ya kumlinda Lipumba
na Kundi lake ikiwemo kufuta kesi zilizofunguliwa na Bodi ya Wadhamini
ya chama hicho dhidi ya mwenyekiti huyo anayetambuliwa na Ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa na wenzake ambazo zimelenga kukilinda chama
hicho.
Hali
kadhalika amesema kuwa, CUF imekwisha pitia migogoro mingi ambayo chama
hicho imeshinda kwa kuwa ni taasisi imara na kudai kwamba mgogoro
uliopo sasa haujalenga kukisambaratisha chama hicho pekee bali umelenga
kuiua demokrasia nchini kwa kukandamiza na kuzuia taasisi za
kidemokrasia Tanzania kutekeleza majukumu yake.
“Huu
ni wakati wa wapenda demokrasia na wapenda amani wote kusimama pamoja
kuilinda demokrasia na taasisi zetu zinazohamasisha demokrasia,” alisema.

No comments