SERIKALI KUENDELEA KUTOA DAWA YA KUTIBU SUMU YA NYOKA
SERIKALI imesema itaendelea kutoa dawa
zinazotibu sumu ya nyoka ili kupambana na tatizo hilo nchini. Kauli hiyo
ya serikali ilitolewa Dar es Salaam jana na Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
“Kama tunavyofahamu nchi yetu ina aina
mbalimbali za nyoka ambao pindi wakimuuma mtu huleta madhara mbalimbali
ya kiafya. Aidha tunafahamu kwamba tatizo hili lipo zaidi katika maeneo
ya vijijini ambako uwezo wa wananchi kumudu gharama za matibabu ni
mdogo.”
Alisema dawa za kutibu sumu ya nyoka
huagizwa kutoka nje ya nchi; na kwamba si tu hazipatikani kwa urahisi,
bali pia zinapatikana kwa gharama kubwa.

Waziri huyo alisema bei ya kununulia
dawa hizo ni kati ya dola za Marekani 55 hadi 85 (yaani Sh 118,250 hadi
182,750) kwa kichupa kidogo kimoja.
Alisema kichupa hicho huweza kutumika
kwa wagonjwa wanne, lakini mara tu baada ya kufunguliwa dawa hiyo huwa
haifai tena kutumika ndani ya mwezi mmoja tu.
Waziri alisema pamoja na changamoto
hizo, Serikali kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kila mwaka huagiza dawa
hizo kwa ajili ya mahitaji hayo ya kutibu wagonjwa walioumwa na nyoka,
ambapo bei ya kuinunua kutoka MSD ni Sh 200,000 kwa kichupa kimoja.
“Hospitali zetu mbalimbali zimekuwa
zikiagiza dawa hizi kutoka MSD na kwa wasambazaji wengine kwa bei hii au
zaidi na kuwatibu waathirika wanaohitaji dawa za sumu za nyoka mara
zinapohitajika. “Napenda kuwakumbusha kwamba kwa mujibu wa Sera ya Afya
ya mwaka 2007, huduma za tiba hutolewa bure kwa makundi maalumu au kwa
kuchangiwa kwa sehemu ya gharama, au kwa kupitia mfumo wa bima
mbalimbali za afya kama vile CHF.
“Kwa wale wasio na uwezo na wanaothibitishwa kuwa hawana uwezo, utaratibu wa msamaha hutumika,” alisema Waziri.
Alisema katika kuhakikisha kwamba
wananchi wanaohitaji dawa ya sumu ya nyoka wanahudumiwa ipasavyo,
waganga wakuu wa mikoa na viongozi wa hospitali zote nchini, wanatakiwa
kuhakikisha hospitali zote za umma zinaingiza dawa hiyo katika dawa za
dharura ili iweze kununuliwa kama dawa zingine za dharura kupitia
kifungu cha fedha za dawa za dharura.
No comments