NSSF Yaburuzwa Mahakamani
SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), limeburuzwa mahakamani na wakazi 87 waliokopeshwa nyumba za mradi wa shirika zilizoko Kijichi jijini Dar es Salaam, wakiiomba lisiwabugudhi hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa.
Kesi
hiyo imefunguliwa na wakazi hao katika Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi,
wakilalamikia Bodi ya Wakurugenzi ya NSSF na Kampuni ya Majembe Auction
Mart.
Kesi hiyo ilipangwa kutajwa jana mbele ya Jaji Penterine Kente.
Wakili
wa walalamikaji hao, Benito Mandele, amewasilisha maombi mahakamani
hapo kutaka itoa amri ya kutokubugudhiwa na mazingira ya makazi hayo
yabaki kama yalivyo hadi kesi yao ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa
uamuzi.
Katika
kesi ya msingi, mbali na NSSF, mlalamikiwa wa pili ni Majembe ambaye
hakufika mahakamani. Wakili Mandele alidai kuwa alipeleka wito wa
mahakama katika ofisi yake iliyoko Mwenge, lakini hakufanikiwa kumpata
kwa kuwa amehamisha ofisi eneo hilo.
Jaji
Kente alisema mahakama inatoa hati nyingine kwa ajili ya mlalamikiwa wa
pili ili afike mahakamani kusikiliza kesi dhidi yake.
Kesi ya msingi itasikilizwa Oktoba 17, mwaka huu, na maombi ya
kutokubughudhiwa yatasikilizwa Agosti 24, mwaka huu.
Wakazi
hao kupitia kwa wakili wao, waliamua kukimbilia mahakamani kufungua
shauri hilo, baada ya kushindwa kupata ufumbuzi wa madai yao katika
Taasisi ya Usuluhishi kutokana na walalamikiwa kutofika.
Ilidaiwa
kuwa wakazi hao waliamua kwenda katika taasisi ya usuluhishi kutokana
na mkataba wao kuwataka kufanya hivyo kabla ya kuamua kwenda
mahakamani.
Kwa
mujibu wa hati ya madai, wakazi hao wanadai kwamba mlalamikiwa wa
kwanza (Bodi ya Wakurugenzi ya NSSF), ameshindwa kutekeleza makubaliano
kwa mradi huo kukosa huduma za kijamii.
Aidha, wanadai nyumba hizo hazina ubora hali iliyowalazimu wengi wao kutumia fedha zao kufanya ukarabati.
Wanadai
kuwa kutokana na hali hiyo, baadhi ya wakazi wameshindwa kulipa fedha
ambazo wanatakiwa kulipa kila mwezi, hivyo Majembe walifika na kuwapatia
notisi na kuwatangazia kuwaondoa.
Wakazi
hao wanaiomba mahakama hiyo, kuiamuru bodi hiyo kurejea mikataba,
kutambua majukumu ya msingi ya kila upande na nyumba ziwe za kuwawezesha
kuishi na kuwe na huduma za kijamii.
Katika
maombi, wakazi hao wanaiomba mahakama hiyo kutoa amri ya hali ilivyo
kwa wakazi hao katika makazi hayo ibaki kama ilivyo mpaka kesi ya msingi
itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.