VITAMINI A NA UMUHIMU WAKE
Vitamini ni virutubisho vya lishe vipatikanavyo katika vyakula mbalimbali, na virutubisho hivi ni muhimu katika kusaidia mwili katika utendaji kazi wa mifumo mbalimbali . Kuna makundi mawili ya vitamini. Moja ni kundi la vitamini zinazochanganyika katika maji nazo ni vitamini B na vitamini C, na pili ni aina za vitamini zinazochanganyika katika mafuta nazo ni A,D,E na K.Vitamini A ni kundi la vitamini inayochanganyika katika mafuta, na vitamini hii hujulikana pia kama retinol, retinal,retinoic acid na beta-carotene; na katika yote hayo beta carotene ndiyo iliyo muhimu zaidi.
Kirutubisho hiki ni muhimu kwa ukuaji na afya bora, ambapo huimarisha kinga ya mwili na husaidia afya ya macho na kuona vyema. Vitamini A hutusaidia kuepukana na upofu wa kuona usiku,pia husaidia kuona vyema nyakati za mchana. Beta carotene ni muhimu kwa sababu huondoa sumu mwilini zijulikanazo kama free radicals, na hii ni ile
Beta carotenoidi inayopatikana katika vyakula na siyo ile inayopatika katika virutubisho vya dukani, na imeonekana kupunguza uwezekano wa kupata maradhi ya kansa. Vitamini hii pia husaidia afya ya seli,tishu, ngozi,meno na mifupa.
Vitamini A hupatikana katika vyakula vitokanavyo na wanyama kama, Mafuta ya samaki, maini,figo, maziwa,jibini na samaki. Maziwa yaliyoondolewa siagi huwa hayana vitamini A, labda kama itaongezewa na wasindikaji.
Beta carotinoidi hupatikana katika vyakula vya asili ya mimea kama, Matunda ya njano kama machungwa,papai,embe,tipisi(pitches) na zabibu za pink. Pia vitamini hii hupatikana katika mboga kama, karoti,maboga,viazi vitamu, majani vya viazi vitamu (tembere),pilipili na spinachi. Kwa kawaida rangi ya njano ya matunda na mbogamboga iliyokoa sana inaashiria uwepo kwa wingi wa beta carotinoidi.
Upungufu wa vitamini A, husababisha kutokuona usiku, ukavu wa macho kwa kushindwa kutengeneza machozi, upofu,ngozi kavu, kupoteza uwezo wa kunusa na kukosa hamu ya kula. Upungufu wa vitamini hii husababisha mtu kuwa na kinga dhaifu hivyo kushambuliwa na maradhi.
Vitamini A huchanganyika vyema na mafuta, vyakula vyenye vitamini A vitafyonzwa vyema mwilini endapo vitapikwa kwa kutumia mafuta.
Epuka kutumia vitamini A kutoka virutubisho vya kununua dukani bila ushauri wa mtaalamu wa lishe au daktari, pata ushauri wa mfamasia dhidi ya matumizi bora ya Vitamini A. Dozi kubwa za vitamini A kutoka katika virutubisho vya dukani zaweza kukuletea madhara.
Njia nzuri ya kujipatia vitamini A, ni ulaji wa aina tofauti za matunda, mbogamboga na vyakula vingine tulivyoviona hapo awali.
No comments