JE NI MUHIMU KUFAHAMU AINA YA KUNDI LA DAMU YAKO?
Binadamu tumeumbwa na aina tofauti za damu, zijulikanazo kama makundi ya damu. Aina hizi za damu zimegawanyika katika mifumo mikuu miwili, ambayo ni:
Mfumo wa makundi ABO.
Mfumo Rh (Rhesus).
Makundi ya damu zetu hutambuliwa kutokana na aina za jeni tunazorithi kutoka kwa wazazi wetu. Kwa hiyo kundi la damu yako hujulikana kutokana na aina zifuatazo za dutu zipatikazo katika damu yako:
Antijeni- ni aina ya protini ipatikanayo juu ya uso wa seli hai nyekundu ya damu, na husababisha utengenezwaji wa kingamwili.
Kingamwili- hii ni protini ambayo hupambana na maambukizi ya magonjwa, ambayo hupatikana katika plasmadamu ( maji ute ambayo ni sehemu ya damu). Kingamwili ni sehemu ya mfumo wa kinga mwilini, ambayo huzishambulia aina maalum za antijeni zinazoingia kwenye damu yako(mfano kwa kuongezewa damu isiyolandana na damu yako).
Mfumo ABO- Katika mfumo huu, damu yako yaweza kuwepo katika mojawapo ya makundi manne yafuatayo:
Kundi A - Unayo antijeni A kwenye uso wa seli hai nyekundu za damu, na kingamwili kinga-B (ambayo huzishambulia antijeni B).
Kundi B -Unayo antijeni B kwenye uso wa seli hai nyekundu za damu, na kingamwili kinga-A (ambayo huzishambuli antijeni A).
Kundi AB- Unayo antijeni A na B na kingamwili kinga A na kinga B.
Kundi O -hauna antijeni katika uso wa seli hai nyekundu ya damu, lakini unayo kingamwilikinga A na kinga B.
Mfumo wa Rh- Seli hai nyekundu za damu zaweza pia kuwa na aina nyingine ya antijeni zijulikanazo kama RhD (Rhesus factor).
RhD chanya (Rhesus positive)-ambayo inayo antijeni.
RhD hasi (Rhesus negative)-ambayo haina antijeni.
Walio wengi katika Afrika ya mashariki ni RhD chanya. Kwa hiyo basi, kundi la damu yako hutambuliwa kwa kuangalia mfumo ABO pamoja na RhD. Kwa mfano, kama damu yako ni kundi O pamoja na RhD chanya, basi kundi lako la damu litatambulika kama O chanya (O positive).
Damu ya kundi O ndiyo iliyo adimu zaidi katika benki za damu, hii ni kwa sababu aina O ndiyo aina ambayo yaweza kuwekewa kwa mgonjwa wa kundi lolote la aina za damu.(universal donor)
Kwa nini kufahamu makundi ya damu ni muhimu?
Wataalam wa afya, hawana budi kuichunguza damu ya mgonjwa kabla ya kumuongezea damu kutoka kwa mtu mwingine ambaye atachangia damu hiyo. Baadhi ya makundi ya damu huwa hayaendani. Mfano, kama mgonjwa ana kundi la damu aina A, haiwezekani kumuwekea damu kutoka aina B, hii ni kwa sababu kingamwili kinga B ya damu ya mgonjwa itaishambulia antigeni B ya damu ya damu kutoka kwa mchangiaji. Makosa ambayo hutokea wakati wa kumuwekea mgonjwa damu isivyo sahihi huwa ni nadra, lakini endapo itatokea, basi maisha ya mgonjwa huwa hatarini.
Wakati wa dharura, itakuwa msaada mkubwa endapo kundi la damu ya mgonjwa litajulikana mapema ili kuweza kuokoa maisha ya mgonjwa. Kujua kundi lako la damu, kutawasaidia wataalam wa afya kuweza kufanya utafiti wa haraka zaidi ili kuweza kukupatia msaada wa haraka wakati wa dharura itayohitaji matibabu ya kuwekewa damu.
Nitawezaje kufahamu aina yangu ya damu?
Waweza kufahamu aina ya kundi lako la damu endapo utaenda kuchangia damu. Pia endapo utakuwa unahitajika kuongezewa damu, itabidi aina ya damu yako ifanyiwe utafiti wa maabara ili kujua .Lakini pia waweza kwenda maabara kwa ajili kwa ya vipimo na kuweza kujua aina ya kundi la damu yako.

No comments