HUENDA HARUFU YA KUKU IKAWA SULUHISHO LA KUZUIA MALARIA-UTAFITI
Harufu ya kuku aliye hai inaweza siku moja kuwa suluhisho la kupambana na maradhi hatari ya malaria, ambayo husababisha idadi kubwa ya vifo kila mwaka ulimwenguni kote. Hii ni kwa mujibu wa shirika la habari la BBC.
Katika utafiti uliofanywa na wanasayansi wa Ethiopia na Uswidi, watafiti hao wamegundua kuwa mmbu waenezao malaria huwa hawapendi
harufu ya kuku na ndege wengine. Katika utafiti huo uliofanyika huko magharibi mwa Ethiopia, ulihusisha kumweka kuku katika kiota cha kuning'inia ndani ya chumba karibu na mtu wa kujitolea alipokuwa analala lakini alikuwa anatumia chandarua.
Utafiti huo ambao ulichapishwa katika jarida la tafiti za malaria, wanasayansi hao walihitimisha kuwa, kwa kuwa mmbu hutumia harufu ili kuwafikia wanyama ambao huwanyonya damu, huenda kuna aina ya dutu itoayo harufu isiyowapendeza mmbu hao kutoka viumbe aina ya ndege na kusababisha mmbu kukaa mbali kuku.
Mmoja wa watafiti aliyehusika kutoka chuo kikuu cha Addis Ababa alisema kuwa "Dutu hiyo yaweza kutengwa kutoka kwa ndege na inaweza kutumika kutengeneza dawa za kufukuzia mmbu".
Watafiti wanasema kuwa utafiti huu ni muhimu kwa kuwa mmbu wameanza kujenga usugu dhidi ya aina nyingi za viwatilifu vinavyopatikana nyakati hizi.

No comments